Maswali na majibu baada ya Gödel na Turing

Neno sayansi linatokana na neno “scio” la kilatini lenye maana ya kujua ama kufahamu. Hivyo basi, masomo yote yanayochukuliwa kuwa aina ya sayansi yanajihusisha na kutafiti ukweli wa mambo – iwe ni kwa kufanya majaribio (ambapo inakuwa sayansi tendeshi) au kwa kukisia kanuni za ukweli na kuzithibitisha (ambapo inakuwa ni sayansi nadharia).

Nitakayoyazungumzia hapa ni historia fupi ya utafiti wa sayansi ya kompyta, haswa maswali yaliyoanzisha usomi huu. Kwa watu wengi, masomo ya tarakirishi huchukuliwa kuwa miongoni mwa masomo ya uhandisi. Ni kweli kwamba sehemu nyingi za somo hili zinazojihusisha na kifaa tarakirishi chenyewe – iwe ni hadweya au softweya ya vifaa – na sehemu hizi huwa ni uhandisi. Lakini pia, somo hili linajihusisha na mengi zaidi ya haya – ukiangalia asili la neno kompyuta utapata linatokana na neno “compute” la kiingereza ambalo lina maana ya “kupata jibu, hasa kwa swali la hisabati, kwa kutumia kanuni fulani”[1] . Tutakavyoona sayansi hii inahusika na maswali ya muundo wa “Je swali hili linajibika kwa kufuatia kanuni?”,”Linahitaji kanuni ngapi?” n.k. Read more