‘Sikate Tamaa ni jina la diwani ya kwanza ya mashairi ya Said Ahmed Mohammed. Niligundua diwani hii siku moja maktabani nilipokuwa kidato cha tatu. Kilichonivutia kwanza ilikuwa ni muundo wa mashairi ya diwani hii – mengi yalikuwa mafupi na, tofauti na nilivyozoea, ni machache tu yaliyokuwa tarbia. Nilianza kusoma shairi la kwanza huku nikijitayarisha kukumbana na misamiati.

Shairi lenyewe lilitirirka – maneno pia na mawazo. Hili lilikuwa shairi lililopendeza kusoma, lenye maudhui dhabiti na lenye lugha isiyoficha maana. Halikuvunja urari wa vina au kanuni zingine zilizotawala ushairi – idadi ya vina katika kila mshororo. Hii ilikuwa ndio sanaa iliyokamilika.

Ilikuwa ndio mara yangu ya kwanza kupata shairi la kiswahili lililopendeza hivi. Baada ya kusoma mashairi mawili au matatu yaliyofuatia nilijua kwamba lazima ningenua kitabu hiki. Malenga huu alipata mfuasi.

Shairi hilo la kwanza, ‘Sikate Tamaa, limenipa moyo mara nyingi pale nilipokaribia kufa tamaa.

Umeanguka, inuka, simama kama mnazi
Umechunika, inuka, tia dawa kwa ujuzi
Sasa inuka, inuka, kijana ianze kazi
Sikate tamaa

Usife tamma, nyanyuka, ni muweza wa kutenda
Kuna hadaa, nyanyuka, anza tena kujipinda
Dunia baa, nyanyuka, anza tena kujiunda
Sikate tamaa

Sivunjwe moyo, dunia, hivyo itakunyanyasa
Futa kiliyo, dunia, hiyo idhibiti sasa
Ipe kamiyo, dunia, kamwe, siache kufusa
Sikate tamaa

Una nguvu, simama, wewe upambane nao
Una werevu, simama, uzepuke njama zao
Usiche kovu, simama, ujifunze vumilio
Sikate tamaa

Shairi hili ni aina ya tarbia lakini si tarbia ya kawaida. Ingawa kila ubeti una mishororo minne, tunapata kwamba kila mshororo umegawa kwa vipande vitatu badala ya kawaida ya vipande viwili. Vipande vyenyewe bado vinadhihirisha urari wa vina na kipande cha kati kinarudiwa kwa kila ubeti. Kurudia huku kunachangia utamu/ladha ya shairi kwani kuna usawa fulani. Pia kurudia huku kunahimiza ujumbe wa shairi hili.

Ushairi wa Said Ahmed Mohamed umenielimisha na kunisisimua tangu niliposoma diwani yake ‘Sikate Tamaa nikiwa shule ya upili. Nilipozidi kutafiti nilipata kwamba mashairi yake yametumika katika mitihani ya kitaifa ya Fasihi mara si haba. Nilipofanya mtihani wangu 2001, tulitahiniwa “Nimeona”, shairi linalotoka kwa diwani hii.

Sina uhakika kuhusu kipindi cha ‘copyright’ cha mashairi haya lakini nitachukua kwamba ni sawa kutumia shairi hili kuelimisha. Hapa basi, ni shairi “Si Dunia ya Kulala” kutoka kwa diwani hii.

Umelala, bado umelala, huamki kwani?
Una dhila, bado una dhila, zitatoka lini?
Pa kulala, bado pa kulala, hujapabaini
Na chakula, hata na chakula, pia wakuhini
Si dunia ya kulala.

Naujuwe, wewe naujuwe, ndiwe mdhamini
Kama siwe, wewe kama siwe, ni dhiki baini
Jipekuwe, wewe jipekuwe, muhimu yakini
Uyajuwe, wewe uyajuwe, utoke gizani
Si dunia ya kulala